Viongozi wa Kiislamu Kenya walaani hatua ya Trump dhidi ya Quds
Viongozi wa Kiislamu nchini Kenya wamelaani uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kuutangaza mji wa Baitul Muqaddas wa Palestina kuwa mji mkuu wa utawala pandikizi wa Israel.
Wakiongozwa na Sheikh Abubakar Bini, Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu nchini humo CIPK tawi la Bonde la Ufa, viongozi hao wamesema kitendo hicho cha Trump hakitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kushadidisha taharuki na machafuko katika eneo la Mashariki ya Kati.
Amesema, na hapa tunanukuu: "Tumehuzunishwa sana na hatua ya Trump ya kuitambua Jerusalem (Quds tukufu) kuwa mji mkuu wa Israel. Hatua hiyo haifai na inaonyesha kutowajibika kwa Trump, na ni kitendo ambacho kinafaa kupingwa kwa nguvu zote." Mwisho wa kunukuu.
Dakta Sheikh Jamal Mungatana, kiongozi na mwanaharakati mashuhuri nchini Kenya naye amesema hatua hiyo ya Trump itakuwa na taathira hasi, huku akimtaka rais huyo wa Marekani aghairi msimamo huo wa kichochezi.
Kadhalika ameitaka jamii ya kimataifa ifuate mafundisho ya Vitabu Vitakatifu na isimame dhidi ya viongozi mfano wa Trump wanaodhalilisha dini na madhehebu nyingine.
Uamuzi huo wa Rais wa Marekani wa kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kuagiza kuanzishwa mchakato wa kuuhamishia ubalozi wake mjini humo kutoka Tel Aviv unaendelea kulaaniwa kote duniani na hata waitifaki wa Washington kama vile Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na hata nchi za Kiarabu.