Sudan: Hatutaitambua mipaka mipya ya majini iliyowekwa na Misri na Saudia
Sudan imewasilisha taarifa kwa Umoja wa Mataifa ikieleza kwamba endapo mipaka mipya ya majini iliyowekwa na Misri na Saudi Arabia itapitishwa rasmi haitoitambua katu mipaka hiyo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imewasilisha taarifa kwa Umoja wa Mataifa na kutangaza kuwa inapinga makubaliano yaliyofikiwa kati ya Misri na Saudia ya kuchora mipaka mipya ya majini kufuatia makubaliano ya pande mbili ya mwaka uliopita wa 2016.
Katika taarifa yake hiyo kwa Umoja wa Mataifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesisitiza kuwa katika makubaliano hayo eneo la Pembe Tatu la Hala'ib (Hala'ib Triangle) ambalo linagombaniwa na Sudan na Misri limetambuliwa kuwa ni sehemu ya ardhi ya Misri.
Taarifa hiyo aidha imefafanua kuwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa na makubaliano ya Vienna ya mwaka 1969, Khartoum inatangaza wazi kwamba haibebi dhima yoyote kisheria kuhusu makubaliano ya kuweka mipaka mipya ya majini yaliyofikiwa kati ya Misri na Saudi Arabia.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan aidha imesisitiza kwamba makubaliano hayo yanakiuka haki za Sudan kwa eneo la pembe tatu la Hala'ib.
Itakumbukwa kuwa katika safari iliyofanywa na Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudi Arabia nchini Misri mwezi Aprili mwaka jana, Cairo na Riyadh zilisaini makubaliano ambayo yalipelekea Misri kuipatia Saudia visiwa viwili vya Tiran na Sanafir.
Vyama na makundi ya kisiasa nchini Misri yalifanya maandamano makubwa ya kupinga na kulalamikia uamuzi huo yaliyoulaani vikali na kuueleza kuwa ni uhaini na usaliti dhidi ya taifa la Misri. Uamuzi huo wa serikali ya Cairo ulibatilishwa pia na Mahakama Kuu ya Kiidara ya nchi hiyo.../