Macron: Ufaransa ipo tayari kuimarisha uwepo wake kijeshi katika eneo la Sahel
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema kuwa nchi yake ipo tayari kuimarisha uwepo wake kijeshi katika eneo la Sahel barani Afrika ili kushirikiana na vikosi vya Kiafrika katika mapambano dhidi ya wanamgambo wenye misimamo mikali katika eneo hilo.
Akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari huko Niamey mji mkuu wa Niger na mwenzake wa nchi hiyo Rais Mahamadou Issoufou, Rais Macron alisema kuwa Ufaransa ipo tayari si tu kwa ajili ya kudumisha lakini kuimarisha uwepo wake kijeshi huko Sahel kama italazimika kwa sababu mapambano dhidi ya ugaidi katika eneo hilo yana umuhimu kwa mtazamo wake. Rais Macron ameyasema hayo ikiwa zimepita siku chache licha ya mipango ya huko nyuma ya Ufaransa ya kutaka kuondoa vikosi vyake huko Sahel kwa msaada wa kikosi kipya cha kijeshi cha Kiafrika kijulikanacho kama (G5 Sahel).
Kikosi hicho cha kijeshi kinachowajumuisha wanajeshi kutoka Mali, Niger, Chad, Burkina Faso na Mauritania kilianza oparesheni zake rasmi mwezi Novemba. Kikosi hicho kimepanga kuendesha doria katika eneo la Sahel kwa kushirikiana na wanajeshi 4000 wa Ufaransa waliotumwa katika eneo hilo.