Ethiopia yakamata watu 107 waliohusika na ghasia
Serikali ya Ethiopia imewatia mbaroni watu 107 kwa tuhuma za kuhusika na vurugu zilizotokea hivi karibuni kwenye eneo la mpaka wa mikoa ya Somali na Oromia.
Kamishna wa tume ya polisi ya Ethiopia, Abiyu Assefa amesema, watuhumiwa 98 kati ya hao waliokamatwa wanatokea mkoa wa Oromia na wengine tisa ni kutoka mkoa wa Somali.
Mapigano makali katika eneo la mpaka wa mikoa hiyo miwili ya Ethiopia ambayo yalitokea mwezi Septemba mwaka jana yalizusha mapigano ya kikabila yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa na mamia ya watu kukimbia makazi yao.
Machafuko katika eneo la Oromia yalianza mwaka 2015 baada ya kutekwa ardhi za wakulima na matajiri wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Wakaazi wa eneo hilo wanailaumu serikali ya Addis Ababa wakidai kuwa ndiyo iliyowasaidia mabepari na mabwanyenye kupora ardhi zao kama ambavyo walilalamikia pia ukandamizaji wa kisiasa wanaofanyiwa na serikali hiyo.
Aidha wanataka serikali ifanye marekebisho ya kisiasa na kijamii ikiwa ni pamoja na kukomesha uvunjaji wa haki za binadamu hususan mauaji ya raia, kutiwa mbaroni makundi kwa makundi ya watu na kutengwa kisiasa wapinzani wa serikali.