Sudan yafunga mpaka na Eritrea, yatuma maelfu ya askari mpakani
Sudan imetangaza rasmi kufunga mpaka wake na Eritrea baada ya kutuma maelfu ya wanajeshi katika jimbo la Kassala lililopo katika mpaka wa Eritrea.
Gavana wa jimbo la Kassala, Adam Jamma ameagiza kufungwa kwa mipaka yote na Eritrea, ikiwa ni utekelezaji wa tangazo la hali ya hatari lililotolewa na Sudan hivi karibuni katika jimbo hilo.
Uamuzi huo umeweka sharti la kufungwa mipaka yote na Eritrea kuanzia jioni ya Januari 5 mwaka 2018 hadi taarifa zaidi itakapotolewa.
Uamuzi huo unakuja saa chache baada ya Serikali ya Sudan kukanusha kuwepo kwa mgogoro baina yake na Eritrea, na kusema kuwa imesambaza vikosi vyake katika jimbo la Kassala ikiwa ni sehemu ya kutekeleza mfumo wake wa dharura na agizo la kukusanya silaha na magari yasiyosajiliwa, kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu na magendo ya silaha na bidhaa.

Disemba 30 mwaka 2017, Rais wa Sudan Omar al Bashir alitangaza hali ya hatari katika jimbo la Kordofan Kaskazini lililoko magahribi ya Sudan na jimbo la Kassala lililopo mashariki ya Sudan.
Ripoti zaidi zinasema kuwa, Misri, ikiungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu imetuma wanajeshi wake nchini Eritrea. Uhasama baina ya Sudan na Misri umeongezeka hasa baad aya safari ya Rais Recep Tayyip Erdogan’s wa Uturuki nchini Sudan mwezi Disemba. Vyombo vya habari Misri vinaituhumu Sudan kuwa imejiunga na muungano wa Uturuki, Iran na Qatar. Sudan na Misri pia zina mgogoro wa muda mrefu wa mpaka.