Malalamiko yaongezeka dhidi ya serikali nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38977-malalamiko_yaongezeka_dhidi_ya_serikali_nchini_sudan
Malalamiko ya wananchi ya kulalamikia ughali wa maisha na hali ngumu ya kiuchumi yameongezeka nchini Sudan huku kukiwa na tetesi kwamba huenda serikali ya nchi hiyo ikavunjwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 14, 2018 23:47 UTC
  • Malalamiko yaongezeka dhidi ya serikali nchini Sudan

Malalamiko ya wananchi ya kulalamikia ughali wa maisha na hali ngumu ya kiuchumi yameongezeka nchini Sudan huku kukiwa na tetesi kwamba huenda serikali ya nchi hiyo ikavunjwa.

Hayo ni kwa mujibu wa gazeti la al Hayat ambalo limeripoti kuwa, maandamano ya wananchi wa Sudan ya kulalamikia kupanda bei za bidhaa muhimu na huduma za umma yameongezeka sana nchini Sudan na kuna hatari ya kuvunjika serikali ya umoja wa kitaifa ya Waziri Mkuu, Bakri Hassan Saleh.

Maandamano nchini Sudan

 

Kwa mujibu wa gazeti hilo, Rais Omar al Bashir wa Sudan anafikiria kuivunja serikali ya Waziri Mkuu Bakri Hassan Saleh kutokana na kushindwa kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi na kupanda bei za bidhaa muhimu kama mkate na umeme na hali mbaya ya kushuka thamani sarafu ya nchi hiyo.

Maandamano yameenea Sudan nzima kulalamikia hatua ya serikali ya kupandisha bei za bidhaa hizo muhimu. Hadi hivi sasa mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari ameshauawa na watu wengine sita wameshajeruhiwa katika maandamano hayo.