Sudan yasema inakabiliana na tishio katika mipaka yake na Misri, Eritrea
Serikali ya Sudan imesema inakabiliana na tishio la usalama katika mipaka yake na nchi jirani za Misri na Eritrea.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ibrahim Ghandour aliyasema hayo Jumapili mjini Khartoum akihutbia kikao cha waandishi habari akiwa ameandamana na mwenzake wa Ethiopia Workneh Gebeyehu. Aidha amesema kuwa wamegundua kuwa kuna nchi inayojaribu kuwadhuru na kwamba jeshi la Sudan limepanga upya vikosi vyake ili kukabiliana na kitendo chochote kitakachoharibu usalama wa Sudan.
Kwa upande wake Bw. Gebeyehu amesema, Ethiopia inapenda kukuza uhusiano wa pande mbili kati yake na Sudan, na kuendelea kusaidia kuhimiza amani katika kanda hiyo.
Kauli hiyo inakuja baada ya kuenea ripoti kuwa Misri, ikiungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu imetuma wanajeshi wake nchini Eritrea. Kufuatia taarifa hizo wiki iliyopita Sudan ilitangaza rasmi kufunga mpaka wake na Eritrea baada ya kutuma maelfu ya wanajeshi katika jimbo la Kassala lililopo katika mpaka wa Eritrea.
Pamoja na hayo, Rais Isaias Afwerki wa Eritrea amekanusha kuwepo askari wa Misri nchini humo. Aidha amezituhumu Sudan na Ethiopia kuwa zinataka kuitumbukiza nchi yake katika vita huku akisema dalili ya njama hiyo ni kuwepo idadi kubwa ya askari wa Sudan katika jimbo la Kassala.
Hali kadhalika Rais wa Eritrea amesema ni jambo lisilokubalika kwa askari wa Uturuki kuwepo katika eneo la Bahari ya Sham na katika nchi ya Somalia akidai kuwa jambo hilo litavuruga uthabiti wa kieneo. Ametoa tamko hilo baada ya Rais Reccep Taayib Erdogan wa Uturuki kutembelea Sudan mwezi Disemba ambapo Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo alitoa idhini ya kujengwa kituo cha kijeshi cha Uturuki katika kisiwa cha Saukin cha Bahari ya Sham.