UN yapinga tena uamuzi wa Marekani wa kuhamishia ubalozi wake Quds tukufu
Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kimesisitiza tena upinzani wa jamii ya kimataifa dhidi ya uamuzi wa Marekani wa kuhamishia ubalozi wake katika mji mtakatifu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na Israel.
Wanadiplomasia walioshiriki katika kikao hicho kujadili hali ya Mashariki ya Kati kwa mara nyingine tena wameeleza upinzani wao dhidi ya uamuzi wa Marekani wa kuhamishia ubalozi wake Quds (Jerusalem) kutoka Tel Aviv.
Kikao hicho cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia kimejadili uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kukata misaada ya nchi hiyo kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa Wakimbizi wa Palestina (UNRWA).
Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Is'haq Aal Habib amesema kuwa chanzo cha migogoro yote ya Mashariki ya Kati ni uvamizi wa Israel na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina na vilevile dhulma za miongo saba ya siasa za kupenda kujitanua na ubaguzi wa utawala huo wa Kizayuni.
Itakumbukwa kuwa tarehe 6 Disemba mwaka jana Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa Washington inaitambua Quds (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa Israel na kwamba itahamishia ubalozi wake katika mji huo kutoka Tele Aviv. Uamuzi huo umepingwa jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Ulaya.
Baada ya hapo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio likitangaza kuwa haliitambui Quds (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa Israel.