Feb 08, 2018 13:54 UTC
  • Kiongozi wa Boko Haram asema amechoka na anatamani kufa

Katika kile kinachoonekana ni kupoteza matumaini na kuhisi kufikwa na maji shingoni, kiongozi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram, Abubakar Shekau amesema amechoshwa na misukosuko na anatamani kufa.

Kwenye kanda ya video ya dakika kumi hivi aliyoitoa jana, Shekau amesema, na hapa tunanukuu, "Nimechoshwa na huu mgogoro, natamani nijifie ili nikajipumzikie 'Peponi'. Mwisho wa kunukuu.

Katika sehemu moja ya video hiyo, kiongozi huyo wa Boko Haram hata hivyo anasisitiza kuwa genge hilo liko imara na wala haliwezi kusambaratishwa na kwamba karibuni hivi litapata ushindi.

Shekau ametoa video hii katika hali ambayo, genge hilo la kitakfiri limeshadidisha hujuma zake katika siku za hivi karibuni, shambulizi la hivi karibuni likiwa ni lile la mwezi uliopita katika eneo la Muna Garage, jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa nchi, ambapo watu 12 waliuawa na wengine wasiopungua 48 kujerihiwa. 

Siku chache zilizopita, Jeshi la Nigeria lilitangaza habari ya kuteka msitu wa Sambisa, ulioko kaskazini mashariki mwa nchi, ambayo ni ngome kuu ya mwisho ya genge hilo la ukufurishaji.

Wanachama wa Boko Haram

Mashambulizi ya Boko Haram yalianza mwaka 2009 nchini Nigeria kwa madai ya kupinga elimu zinazotoka nchi za Magharibi.

Mashambulio ya genge hilo yalipanua wigo wake mwaka 2015 na kuingia pia katika nchi jirani na Nigeria, za Niger, Cameroon na Chad na hadi sasa zaidi ya watu 20,000 wanaripotiwa kuuawa kufuatia mashambulio hayo ya kigaidi ya wanamgambo wa Boko Haram.

Tags