Museveni: Wanaume wanaowapiga wake zao ni wapumbavu
(last modified Thu, 08 Mar 2018 16:25:51 GMT )
Mar 08, 2018 16:25 UTC
  • Museveni: Wanaume wanaowapiga wake zao ni wapumbavu

Nchi za Afrika zimejiunga na ulimwengu katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, huku Rais Yoweri Museveni wa Uganda akiwataja kama wapumbavu, wanaume wanaowapiga wake zao.

Akihutubia taifa katika wilaya ya Mityana katikati ya nchi hii leo, Museveni amesema binafsi ameishi na mkewe Janet kwa zaidi ya miaka 50 lakini hajawahi hata siku moja hata kumsukuma, huku akitoa wito wa kuheshimiwa, kuthaminiwa na kupewa fursa wanawake.

Wakati huo huo, taarifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC kwa mnasaba wa siku hii, imetoa mwito wa kujumuishwa wanawake zaidi katika nyadhifa mbalimbali za uongozi ili kusaidia kufanikisha maendeleo katika nchi sita wanachama.

Moja ya malengo ya EAC ni kuhakikisha wanawake wanapata asilimia 50 ya viti katika nyanja zote za uwakilishi ikiwa ni pamoja na sekta ya siasa, elimu na ajira nyingine kufikia mwaka 2030.

Wanawake wa Kiafrika wakiwa katika shughuli za mapishi

Huku hayo yakiarifiwa, Michael Keating, Mjumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia amewapongeza wanawake wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kwa jitihada zao, ambapo katika miaka ya hivi karibu wamefanikiwa kukwea katika nyadhifa za juu za kisiasa na uchumi wa nchi hiyo.

Amesema wanawake wa Kisomali waliingia kwenye kumbukumbu za historia katika uchaguzi wa mwaka 2016, baada ya asilimia 24 ya wanawake kushinda viti vya bunge, jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa huko nyuma katika nchi hiyo inayokabiliwa na changamoto za kiuchumi na kiusalama.

Tags