Vifo vya Mpox vyapindukia 1,000 huku maambukizi yakienea katika nchi 18 za Afrika
(last modified 2024-10-18T14:00:50+00:00 )
Oct 18, 2024 14:00 UTC
  • Vifo vya Mpox vyapindukia 1,000 huku maambukizi yakienea katika nchi 18 za Afrika

Bara la Afrika wiki iliyopita lilisajili vifo vipya 50 vilivyosababishwa na ugonjwa wa virusi wa Mpox na hivyo kufanya idadi ya watu waliopoteza maisha kwa ugonjwa huo kufikia 1,100 tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Ripoti hii ni kwa mujibu wa takwimu mpya za Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (Africa CDC).

Jean Kaseya, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) ameviambia vyombo vya habari kuwa mwaka huu kituo hicho kimesajili wagonjwa 42,438 wa Mpox katika nchi 18 barani humo. 

Dr. Jean Kaseya 

Wakati huo huo maambukizi mapya 3,051 yalisajiliwa wiki jana huku milipuko mipya mingine ikiripotiwa huko Zimbabwe na Zambia. 

Takwimu za Africa CDC zinaonyesha kuwa asilimia 86.4 ya wagonjwa wa Mpox wanatoka katika Kanda ya Afrika ya Kati.

Wakati huo huo kumekuwa na ongezeko la asilimia 380 za kesi ya ugonjwa wa Mpox mwaka huu ikilinganishwa na mwaka uliopita. 

Mpox ni ugonjwa unaosababishwa na virusi, ambao hapo awali ulijulikana kwa jina la ugonjwa wa tumbili, kabla ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kubadili jina lake mwaka wa 2022 kutokana na malalamiko kwamba jina hilo linaibua hisia za ubaguzi na unyanyapaa.

Ugonjwa huo unaweza kuambukizwa kwa wanadamu kwa kuwasiliana kwa karibu na mtu aliyeambukizwa au na mnyama mdogo wa mwituni, au kupitia vifaa vyenye maambukizi.

Tags