Djibouti imegeuzwa "kambi kuu ya kijeshi ya dunia"
Gazeti la Le Figaro linalochapishwa nchini Ufaransa limeandika kuwa kuwepo utitiri wa wanajeshi wa madola ajinabi nchini Djibouti kumeigeuza nchi hiyo kuwa "kambi kuu ya kijeshi ya dunia".
Makala iliyochapishwa na gazeti hilo imeeleza kuwa katika miongo miwili iliyopita Djibouti imekuwa mithili ya "kambi kuu ya kijeshi ya dunia" na kwamba hivi sasa kuna vituo vitano vya kijeshi vya madola ya kigeni ambayo ni China, Italia, Ufaransa, Marekani na Japan, kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa duniani.
Gazeti la Le Figaro limeeleza katika makala yake hiyo kuwa Djibouti imegeuzwa pia kuwa "pango la majasusi" na kwamba nchi zilizojipenyeza nchini humo kila mmoja inafuatilia nyendo na harakati za nchi nyingine.

Le Figaro limeongeza kuwa kutokana na kuongezeka makundi yanayobeba silaha nchini Somalia, Djibouti imekuwa moja ya nchi zisizo na uthabiti katika eneo la Pembe ya Afrika.
Gazeti hilo limetahadharisha katika makala yake hiyo kuwa, kuzidi kuwepo kijeshi China nchini Djibouti kunaweza kusababisha mikwaruzano kati ya nchi hiyo na nchi za Italia, Ufaransa, Marekani na Japan na kupelekea Djibouti kuwa mlengwa wa makundi yanayobeba silaha nchini Somalia.../