Ujenzi wa ukuta katika mpaka wa Kenya na Somalia wasimamishwa
Shughuli ya kujenga ukuta wa kilomita 700 katika mpaka wa Kenya na Somalia imesimamishwa kwa muda, ili kutoa nafasi ya kufanyika mashauriano zaidi kati ya nchi mbili hizo jirani.
Hayo yamebainika katika mazungumzo kati ya Ali Roba, Gavana wa kaunti ya Mandera iliyoko kaskazini mashariki mwa Kenya karibu na mpaka wa Somalia, na Gavana wa jimbo la Gedo lililoko nchini Somalia, Mohamed A. Mohamed walipokutana leo katika miji ya mipakani ya Mandera na Bulahawa.
Viongozi hao wamebainisha kuwa, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na mwenzake wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmajo wanatazamiwa kukutana karibuni hivi, kuzungumzia masuala kadhaa ambayo yamekuwa na utata na kuhatarisha kuingia doa uhusiano wa pande mbili.
Ujenzi wa uzio huo katika mpaka wa nchi mbili hizo umekuwa ukifanyika kwa mwendo wa kinyonga tangu mradi huo uanze mwaka 2015, baada ya watu 148 aghalabu yao wakiwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Garissa kuuawa katika shambulizi la al-Shabaab, Aprili Pili mwaka huo.
Katika miaka ya hivi karibuni Kenya na Somalia zimekuwa na mivutano ya kisiasa, licha ya serikali ya Nairobi kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiafrika, kutuma askari wake nchini Somalia kwa minajili ya kupambana na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab.
Serikali za nchi mbili hizo zimekuwa na mgogoro juu ya mipaka katika maji ya Bahari ya Hindi, huku Kenya ikikabidhi kwa mashirika ya kigeni haki ya kuchimba mafuta na gesi katika eneo linalogombaniwa. Mbali na hayo serikali ya Mogadishu imekuwa ikilalamikia mpango wa serikali ya Nairobi wa kujenga ukuta wa kilometa 700 katika vijiji vya mpaka wa pamoja wa nchi mbili kwa lengo la kuzuia wanachama wa al-Shabaab kupenya na kuingia nchini Kenya.