Kuimarika uhusiano wa Zimbabwe na China
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42662-kuimarika_uhusiano_wa_zimbabwe_na_china
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amemshukuru rais mwenzake wa China Xi Jinping kwa uungaji mkono wa kisiasa wa nchi hiyo kwa Zimbabwe na kutaka kuimarishwa zaidi uhusiano wa pande mbili.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 05, 2018 01:39 UTC
  • Kuimarika uhusiano wa Zimbabwe na China

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amemshukuru rais mwenzake wa China Xi Jinping kwa uungaji mkono wa kisiasa wa nchi hiyo kwa Zimbabwe na kutaka kuimarishwa zaidi uhusiano wa pande mbili.

Rais Mnangagwa amesema hayo katika ziara yake ya kwanza kabisa ya kuitembelea China tangu aapishwe kuwa Rais wa Zimbabwe mwezi Novemba mwaka jana. Kwa upande wake, Rais Xi Jinping wa China amesema kwamba Zimbabwe ni rafiki wa muda mrefu wa China hivyo anaunga mkono juhudi za kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili katika nyuga zote.

Mnangagwa alianza ziara ya kikazi ya kutembelea China siku ya Jumanne akiongoza ujumbe mzito wa mawaziri 10 na wawakilishi 14 wa sekta binafsi wa nchi yake. Taarifa zinasema kuwa pande mbili zimetilia mkazo suala la kuimarishwa uhusiano wao katika sekta za kiistratijia hasa kilimo, uzalishaji wa tumbaku na uchimbaji wa madini. Wakati huo huo Beijing imeahidi kuwekeza dola bilioni 1 na milioni 400 katika sekta ya uzalishaji umeme nchini Zimbabwe.

Watoto wa Kichina wakishiriki katika sherehe za taifa nchini Zimbabwe

 

Ziara ya Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe huko China ina umuhimu mkubwa hivi sasa. Kwanza ni kwa sababu China ni rafiki wa muda mrefu wa Zimbabwe kiasi kwamba katika miaka ya kuwekewa vikwazo Zimbabwe na nchi za Magharibi, China ilikuwa nchi pekee iliyodhamini mahitaji ya nchi hiyo ya Afrika katika nyuga tofauti za kiuchumi na zana za kijeshi. Ndio maana wachambuzi wa mambo wakasema kuwa, lengo kuu la ziara ya Mnangagwa nchini China hivi sasa ni ya kuishukuru Beijing kwa misaada yake na kuimarisha zaidi na zaidi uhusiano wa pande mbili wa kiuchumi, kisiasa na kijeshi.

China inahesabiwa kuwa ni mshirika wa kiistratijia wa Zimbabwe katika masuala ya kiuchumi. Ahadi kubwa iliyotolewa na Mnangagwa katika sherehe za kula kiapo cha kuwa Rais wa Zimbabwe ilikuwa ni kufufua uchumi wa taifa. Hivyo kuvutia uwekezaji zaidi wa kiuchumi wa Beijing nchini Zimbabwe, ni moja ya malengo makuu ya ziara ya Rais Mnangagwa na ujumbe alioandamana nao huko China. Hii haina maana kwamba hivi sasa hakuna uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo mbili, hapana, bali mashirika ya Kichina yanashiriki kwa nguvu kubwa katika chanjaa tofauti za kiuchumi nchini Zimbabwe. Pamoja na hayo Zimbabwe hivi sasa inasumbuliwa na kuporomoka vibaya uchumi wake, ukosefu wa kazi na ukata wa kupindukia, hivyo inahitajia mno kufufua miundombinu yake ya kiuchumi. Viongozi wa China nao wameonesha wazi kuridhishwa na fursa hizo walizopewa na serikali ya Zimbabwe kwa ajili ya kujitanua zaidi nchini humo ambapo matunda yake hayaishii nchini Zimbabwe tu, bali yanazifikia pia nchi nyingine zote za kusini mwa Afrika. 

Makampuni ya China yamewekeza sana nchini Burundi ikiwa ni pamoja na katika sekta ya uzalishaji tumbaku

 

Jean Joseph Boillo, mtaalamu wa uhusiano wa China na Afrika anaamini kuwa, Beijing ina hamu ya kuona nchi zote za Afrika zinaishi kwa amani bila ya migogoro hususan Zimbabwe kwa sababu nchi hiyo iko katika eneo muhimu la kijiografia huko kusini mwa Afrika na inapakana na nchi kama Msumbiji na Botswana ambazo zina utajiri mkubwa kupindukia wa madini ya almasi. 

Hata hivyo, juhudi za kuimarisha uhusiano wa Zimbabwe na China hazina maana ya kufungwa milango ya kuingia nchi za Magharibi katika nchi hiyo. Ndio maana Mnangagwa akasema kuwa, milango iko wazi kwa nchi za Magharibi kuwekeza nchini mwake. 

Hata hivyo inaonekana kuwa China haifurahishwi sana na kufunguliwa milango kwa washindani wake wa kiuchumi nchini Zimbabwe na mara kwa mara imekuwa ikionesha wazi kuwa haiko tayari kugawana na nchi za Magharibi fursa na manufaa mengi ya bara la Afrika lenye utajiri mkubwa wa maliasili.

Kwa kuzingatia hayo inatabiriwa kuwa, Rais mpya wa Zimbabwe atakuwa na changamoto nzito za kuziridhisha pande zenye ushawishi unaokinzana barani Afrika, ingawa pamoja na hayo inaonekana anastahabu zaidi uhusiano wake na China kuliko nchi za Magharibi ambazo hazina mwamana hata kidogo katika uhusiano wao.