Vikosi vya Mali na Ufaransa vyaua makumi ya magaidi
Jeshi la Ufaransa limetangaza kuwa limeua wapiganaji 30 wa kundi moja la kigaidi nchini Mali kwa kushirikiana na wanajeshi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, karibu na mpaka wa Niger.
Kanali Patrik Steiger amesema leo Alkhamisi kuwa, wanajeshi wa Ufaransa wakishirikiana na wenzao wa Mali wamefanikiwa kuangamiza manachama 30 wa kundi la kigaidi la Jama'a Nusrat ul-Islam wa al-Muslimin (JNIM), lenye mafungamano na genge la ukufurishaji la Daesh (ISIS), kusini mwa mji wa Menaka, karibu na mpaka wa Mali na Niger.
Bila kutoa maelezo zaidi, kamanda huyo wa jeshi la Ufaransa amesema askari kadhaa wa Mali waliuawa pia katika makabiliano hayo ya Jumapili, na kwamba hakuna askari hata mmoja wa Ufaransa aliyejeruhiwa.
Genge hilo la kigaidi lilitagaza kuhusika na shambulio la kigaidi dhidi ya ubalozi wa Ufaransa makao makuu ya jeshi katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ougadougou mnamo Machi 2, ambapo watu wanane waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
Nchi ya Mali inakumbwa na machafuko na mashambulizi ya kigaidi tangu mwaka 2012 wakati yalipotokea mapinduzi ya kijeshi na kuzuka uasi kaskazini mwa nchi hiyo, uliopelekea kutekwa eneo kubwa la nchi hiyo na waasi.
Askari wa Umoja wa Mataifa pamoja na wale wa mkoloni Ufaransa walitumwa nchini Mali katikati ya mwaka 2013, lakini pamoja na hayo wameshindwa kuzima uasi huo na harakati za kigaidi licha ya kukomboa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yametekwa.