Watu 23 wameuawa na kujeruhiwa katika shambulio la silaha kaskazini mwa Mali
Watu 16 wameuawa na wengine saba wamejeruhiwa katika shambulizi la genge moja lenye silaha kaskazini mwa Mali.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Tiéman Hubert Coulibaly, amesema kuwa, shambulizi hilo lilitokea jana usiku wakati kundi moja lenye silaha lilipowavamia na kuwashambulia askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na wanajeshi wa Ufaransa katika mji wa Timbuktu.
Kwa mujibu wa waziri huyo, wanamgambo 15 wenye silaha na afisa mmoja wa kulinda amani wameuawa na wengine saba wamejeruhiwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali ameongeza kuwa magenge ya kigaidi ndiyo yaliyohusika na shambulizi hilo.
Mali imetumbukia kwenye machafuko makubwa tangu mwaka 2012 baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini humo. Baada ya mapinduzi hayo, magenge yenye silaha yalianzisha mashambulizi maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo na kuteka maeneo mengi ambapo hadi hivi sasa yanaendelea kushikilia baadhi ya maeneo hayo.
Mwaka 2013, vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa na vile vya Ufaransa vilitumwa nchini Mali ingawa hata hivyo havijafanikiwa kumaliza mgogoro wa nchi hiyo kiasi kwamba mashambulizi ya magenge ya kigaidi yameongezeka zaidi nchini humo tangu mwaka 2015.