Rais wa Madagascar asema wapinzani wanataka kumpindua
Rais wa Madagascar amewaonya vikali wanasiasa wa upinzani wanaochochea kile anachokitaja kama njama za kumpindua madarakani na kusisitiza kuwa serikali itawachukulia hatua kali za kisheria.
Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Rais Hery Rajaonarimampianina amesema, "Ninawaomba wananchi muwe watulivu na kuheshimu demokrasia. Lakini nisisitize kuwa, kile kilichofanyika Jumamosi ni jaribio la mapinduzi dhidi yangu."
Maelfu ya wapinzani nchini Madagascar waliandamana siku ya Jumamosi katika mji mkuu Antananarivo wakilalamikia sheria mpya za uchaguzi wa Rais zilizopasishwa hivi karibuni na Bunge la nchi hiyo.
Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakipiga nara kupinga sheria mpya za uchaguzi, ambapo wawili miongoni mwao waliuawa huku wengine 16 wakijeruhiwa.
Wapinzani hao wanasema kuwa, sheria hizo mpya zimepasishwa ili kuumzuia mgombea wao Marc Ravalomanana ambaye amewahi kuwa Rais wa nchi hiyo kushiriki katika uchaguzi ujao, uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Marc Ravalomanana alishika madaraka ya Madagascar mwaka 2002 na mwaka 2009 aliondolewa madarakani na aliyekuwa meya wa mji mkuu wa nchi hiyo, Andry Rajoelina, suala ambalo liliitumbukiza nchi hiyo katika machafuko ya ndani yaliyoendelea kwa miaka kadhaa.