May 12, 2018 04:17 UTC
  • WHO yatahadharisha juu ya kuibuka tena ugonjwa wa Ebola huko DRC

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha juu ya uwezekano wa kuibuka tena ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Baada ya ugonjwa wa Ebola kuibuka tena hivi karibuni katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Shirika la Afya Duniani limesema katika taarifa yake kwamba, linajiandaa kwa ajili ya hali mbaya zaidi katika nchi hiyo. 

Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kuwa, mtu mmoja amefariki dunia kwa ugonjwa wa Ebola huku wengine 11 wakithibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo hatari.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Jumatano iliyopita, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitangaza kuwa, kesi mpya za ugonjwa wa Ebola zimeripotiwa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo na kwamba, watu 17 wamefariki dunia.

Hii si mara ya kwanza kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kukumbwa na virusi vya ugonjwa wa Ebola.

Ebola

Ebola iliripotiwa kwa mara ya kwanza nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwaka 1976, wakati huo Zaire na kusambaa katika maeneo mengine ya dunia.

Mnamo mwaka 2014, mlipuko wa ugonjwa huo katika nchi hiyo ulidhibitiwa kwa haraka ingawa watu 49 walifariki dunia.

Itakumbukwa kuwa, watu zaidi ya 11,000 walifariki dunia kutokana na mlipuko wa ugonjwa  wa Ebola katika eneo la Afrika Magharibi mwaka 2014 hadi 2015, hususan nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia katika mlipuko wa Ebola uliotajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani. 

Tags