Ethiopia yakanusha madai ya kuhamishia ubalozi wake Quds Tukufu
Serikali ya Ethiopia imekadhibisha vikali madai kuwa inapanga kuuhamishia ubalozi wake mjini Quds, kutoka Tel Aviv.
Shirika la habari la al-Mayadeen limewanukuu maafisa wa serikali ya Addis Ababa wakiyataja kama uvumi madai kuwa balozi wake wa Tel Aviv alishiriki ufunguzi wa ubalozi wa Marekani katika mji mtukufu wa Baitul Muqaddas na kwamba nchi hiyo ya Kiafrika inajiandaa pia kuuhamishia ubalozi wake katika mji huo wa Palestina unaokaliwa kwa mabavu na Israel.
Meles Alem, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia amesema serikali ya Addia Ababa haina nia wala mpango wowote wa kuuhamishia ubalozi wake mjini Quds kutoka Tel Aviv na kwamba msimamo wao unaenda sambamba na msimamo wa Umoja wa Afrika.
Wakati huo huo, balozi mdogo wa Ethiopia huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu amelaani vikali kitendo cha hivi karibuni cha maafisa wa polisi wa utawala wa Kizayuni wa Israel cha kuwashambulia wafuasi wa Kanisa moja la Kihabeshi lililoko Quds Tukufu, huku Addis Ababa ikitishia kumwita nyumbani balozi wake kutokana na kadhia hiyo.
Itakumbukwa kuwa, Disemba 6, na licha ya makelele na malalamiko ya jamii ya kimataifa, Rais Donald Trump wa Marekani kwa kiburi alichukua uamuzi wa upande mmoja wa kuutambua mji mtakatifu wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, sanjari na kutangaza juu ya kuhamishiwa ubalozi wa Washington mjini hapo kutoka Tel Aviv.