Msafara wa walinda amani wa UN wavamiwa Sudan Kusini, askari auawa
Askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini ameuawa mapema leo Jumanne baada ya msafara wa magari ya mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu kuviziwa na kushambuliwa na genge la wabeba silaha magharibi mwa nchi hiyo.
Duru za habari kutoka UN zimeripoti kuwa, mwanajeshi huyo aliyeuawa katika tukio hilo ni raia wa Bangladesh. Habari zaidi zinasema kuwa, watu kadhaa wamejeruhiwa katika shambulizi hilo lililotekelezwa na genge la wabeba silaha ambalo halijatambuliwa kufikia sasa.
Mwezi uliopita Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) kilituma makumi ya askari wa ziada katika jimbo la Unity ili kuwadhaminia usalama raia wanaolengwa katika vita kati ya askari wa jeshi la serikali na magenge ya waasi.
Shambulizi hilo la leo linajiri siku moja baada ya mazungumzo mengine ya ana kwa ana baina ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na hasimu wake mkubwa Riek Machar kuanza mjini Khartoum na kuhudhuriwa na Rais Omar al Bashir wa Sudan na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kukiwa na matumaini ya kupatikana utatuzi wa vita vya miaka minne na nusu sasa vya Sudan Kusini.

Mazungumzo hayo yamefanyika baada ya mkutano wa siku ya Jumatano iliyopita huko nchini Ethiopia kushindwa kutatua mgogoro huo.
Makumi ya maelfu ya wananchi wameshauwa na karibu milioni nne wengine wamekuwa wakimbizi kutokana na mgogoro na mapigano hayo yaliyozuka mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake wakati huo, Riek Machar kuwa alipanga njama za kumpindua.