Mnangagwa ailaumu G40 inayomuunga mkono Grace Mugabe kwa mripuko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46405-mnangagwa_ailaumu_g40_inayomuunga_mkono_grace_mugabe_kwa_mripuko
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amesema anashuku huenda kundi la G40 linalomuunga mkono Grace Mugabe, mke wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo ndilo lililohusika katika kile anachokitaja kama jaribio la mauaji dhidi yake katika mji wa Bulawayo Jumamosi iliyopita.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 28, 2018 03:31 UTC
  • Mnangagwa ailaumu G40 inayomuunga mkono Grace Mugabe kwa mripuko

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amesema anashuku huenda kundi la G40 linalomuunga mkono Grace Mugabe, mke wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo ndilo lililohusika katika kile anachokitaja kama jaribio la mauaji dhidi yake katika mji wa Bulawayo Jumamosi iliyopita.

Katika mahojiano na shirika la habari la BBC, Mnangagwa hata kama hakumtuhumu moja kwa moja Grace Mugabe, lakini amesema anahisi kuwa kundi la G40 linalounga mkono mpango wa mke huyo wa rais wa zamani wa nchi hiyo kuwania urais ndilo lililohusika na shambulizi hilo.

Rais huyo wa Zimbabwe amesisitiza kuwa hujuma hiyo ilikuwa ya kisiasa na tayari vyombo vya usalama vimewatia mbaroni watuhumwa kadhaa.

Baada ya kujiri mripuko huo katika mkutano wa kampeni za kisiasa mjini Bulawayo, Jonathan Moyo, mwanachama wa ngazi za juu wa kundi la G40, ambaye anaishi uhamishoni na ambaye pia amewahi kuwa waziri katika serikali ya Robert Mugabe aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandano wa kijamii wa Twitter kuwa: "Hii ni kazi ya ndani kwa ndani", akikusudia kuwa mripuko huo uliratibiwa kwa mpangilio maalumu na serikali.

Mnangagwa (kushoto), Mugabe na Grace

Mlipuko huo ulitokea wakati Rais wa Zimbabwe akiondoka uwanjani hapo, baada ya kuwahutubia wafuasi wake, kuelekea uchaguzi mkuu wa Julai 30.

Mtu mmoja alifariki dunia katika mripuko huo wa Jumamosi na wengine wawili wakiripotiwa kuaga dunia juzi, kutokana na majeraha waliyoyapata, huku Rais Mnangangwa akinusurika na makamu wa rais Kembo Mohadi na wengine 48 wakijeruhiwa.

Rais Emmerson Mnangagwa alilitaja shambulizi hilo kuwa la kiwoga na kusisitiza kuwa mbinu hizo katu hazitafuta azma yake ya kuwania urais na kuwahudumia wananchi wa nchi hiyo ya Kiafrika.