Upinzani Djibouti: Kulikuwa na udanganyifu kwenye uchaguzi wa rais
Viongozi wa upinzani nchini Djibouti wametangaza kutotambua ushindi wa Rais Ismail Omar Guelleh katika uchaguzi mkuu uliofanyika Ijumaa iliyopita.
Muhammed Tourtour, mmoja wa wagombea watano wa upinzani katika uchaguzi huo ametaja kama kichekesho na ndoto tangazo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi kwamba Rais Guelleh alishinda kiti hicho kwa asilimia 86 na kusisitiza kuwa, uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu na kasoro nyingi. Omar Elmi Khaireh, ambaye alipata asilimia 7 ya kura zilizopigwa amesema kuna haja ya kufanyiwa marekebisho mfumo wa uchaguzi nchini humo ili kuendana na matakwa ya Wadjibouti walio wengi.
Licha ya vyama vingi vya upinzani kususia uchaguzi huo, lakini Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi imesema kuwa asilimia 68 ya watu laki 1 na 87 elfu waliotimiza masharti ya kupiga kura walijitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo, madai ambayo upinzani unasema kuwa hayaingii akilini. Rais Guelleh mwenye umri wa miaka 68, amekuwa madarakani tokea mwaka 1999.
Djibouti ambayo ni nchi ndogo ya Pembe ya Afrika yenye idadi ya watu wasiofikia hata milioni moja, mwaka 2011 ilishuhudia wimbi la maandamano ya kupinga kuchaguliwa tena Rais Guelleh ambaye ilisemakana kuwa alipata asilimia 80 ya kura zilizopigwa. Maandamano hayo yalijiri baada ya Rais Guelleh kuifanyia marekebisho katiba ya nchi, ili kumruhusu kugombea kiti hicho kwa mara ya tatu mfululizo.