Aug 29, 2018 07:43 UTC
  • Askari waliowapiga na kuwatesa Wabunge wa upinzani Uganda watiwa mbaroni

Askari wa Uganda wanaotuhumiwa kuwapiga na kuwatesa Wabunge wa upinzani akiwemo Mbunge Bobi Wine aliyejizolea umashuhuri wametiwa mbaroni.

Askari hao wametiwa mbaroni siku moja tu baada ya Spika wa Bunge la Uganda Bi Rebecca Kadaga kumwandikia barua Rais Yoweri Museveni akitaka kutiwa mbaroni wanajeshi waliohusika katika kuwapiga na kuwatesa Wabunge.

Miongoni mwa Wabunge wa upinzani ambao walipigwa na kkuteswa na askari walipotiwa mbaroni katika ghasia za kampeni za uchagu mdogo katikka jimbo la Arua ni Bobi Wine ambaye pia ni mwanamuziki.

Bobi Wine ambaye jina lake kamili ni Robert Kyagulanyi na ambaye ni Mbunge wa Kyadondo Mashariki, aliachiliwa kwa dhamana siku ya Jumatatu lakini akiwa katika afya dhoofu pamoja na makovu ya kipigo.

Mbunge Bobi Wine alipokuwa mahakamani hivi karibuni kabla ya kuachiliwa huru kwa dhamana

Mbunge Kassiano Wadri ambaye hivi karibuni alishinda kiti cha Ubunge la Arua amewaambia waandishi wa habari kwamba, alipigwa mara kwa mara na walinzi wa Rais ambao wengine walikua wameficha nyuso zao.

Awali Rais Yoweri Museveni alikanusha habari za kuteswa Wabunge hao na kuvishambulia vyombo vya habari kwa kile alichokisema kuwa, kueneza habari za bandia.

Wapinzani nchini Uganda umeendelea kuilalamikia serikali ya Rais Yoweri Kaguta Museveni kwa kile wanachosema kuwa, ukandamizaji mkubwa dhidi ya wapinzani unaofanywa na vikosi vya usalama vya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Tags