UN: Pande hasimu Sudan Kusini ziliwateka nyara na kuwanajisi mamia ya wanawake
(last modified Wed, 24 Oct 2018 16:49:51 GMT )
Oct 24, 2018 16:49 UTC
  • UN: Pande hasimu Sudan Kusini ziliwateka nyara na kuwanajisi mamia ya wanawake

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini umeeleza kuwa, askari wa serikali na waasi nchini humo wamewateka nyara mamia ya wanawake na wasichana mwaka huu na wengi miongoni mwao walibakwa na kufanywa watumwa wa ngono.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa vitendo hivyo viovu vilifanywa wakati wa vita vya ndani kati ya vikosi vya majeshi ya serikali ya Rais Salva Kiir na wapiganaji wa makamu wa zamani wa rais wa nchi hiyo, Riek Machar.

Umoja wa Mataifa umesema kuwa utekaji nyara huyo umekiuka sheria za kimataifa ni jinai ya kivita. Baadhi ya mabinti waliotekwa nyara na pande hasimu huko Sudan Kusini walikuwa na umri wa miaka 12 tu na walilazimishwa kuwa wake wa askari wa makundi hasimu.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na Makamu wake Riek Machar 

Askari wa pande hizo mbili waliwatumia wasichana hao kama watumwa wa ngono na kuwabaka.

Lul Ruai Koang Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini amekanusha madai hayo. Amesema hakuna uthibitisho unaoonyesha kuwa vikosi vya majeshi ya serikali ya Juba vilifanya vitendo hivyo. Amesema Umoja wa Mataifa unapasa kuonesha ushahidi na si kutoa ripoti tupu kutoka Geneva na New York. 

Naye Paul Gabriel msemaji wa harakati ya waasi wa Sudan Kusini (SPLM-LO) amesema kuwa, uongozi wa harakati hiyo utachunguza tuhuma hizo kupitia njia sahihi na kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria yoyote atakayepatikana na hatia.