Amnesty International yakiri kuuawa kinyama Mashia wa Nigeria
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limevinyooshea kidole cha lawama vikosi vya usalama vya Nigeria likivituhumu kwamba, vimehusika na mauaji ya kinyama ya makumi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo.
Osai Ojigho, Mkurugenzi wa Amnesty International nchini Nigeria ametangaza kuwa, shirika hilo lina ushahidi na nyaraka muhimu zinazoonyesha kwamba, jeshi na vikosi vya usalama vya nchi hiyo viliwafyatulia risasi wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wakati walipokuwa wakiandamana hivi karibuni katika mji mkuu Abuja na viunga vyake.
Taarifa ya Amnesty International imeeleza kuwa, Waislamu 6 wa madhehebu ya Shia waliuawa Jumamosi iliyopita na wengine 39 waliuawa siku ya Jumatatu na vikosi vya usalama vya Nigeria.

Kwa mujibu wa Amnesty international, Waislamu hao waliuawa kinyama mno na vikosi vya usalama vya Nigeria.
Kabla ya hapo pia, Ibrahim Mussa, msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria alikuwa ametangaza kuwa, watu 49 waliuawa shahidi katika matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein AS na katika maandamano yaliyofanyika kwa lengo la kumuunga mkono Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa harakati hiyo anayeshikiliwa na vyombo vya usalama vya nchi hiyo.
Sheikh Zakzaky na mkewe walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati askari wa jeshi la serikali ya Nigeria waliposhambulia Husainiyah ya Baqiyatullah katika mji wa Zaria, jimboni Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo. Siku walipomtia nguvuni Sheikh Zakzaky na mkewe, askari wa jeshi la Nigeria waliwafyatulia risasi waumini waliokuwa wamekusanyika kwenye Husainiyah hiyo na kuwaua shahidi mamia kati yao wakiwemo watoto wake watatu wa kiume.