UN: Watu milioni 2 wanahitaji msaada wa dharura wa chakula CAR
(last modified Thu, 08 Nov 2018 15:49:15 GMT )
Nov 08, 2018 15:49 UTC
  • UN: Watu milioni 2 wanahitaji msaada wa dharura wa chakula CAR

Mpango wa Chakula Duniani WFP umesema watu milioni mbili wapo katika hatari ya kupoteza maisha iwapo hawatafikishiwa msaada wa dharura wa chakula huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Msemaji wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa, Herve Verhoosel amesema leo Alkhamisi kuwa, nchi hiyo ya Kiafrika inakabiliwa na hali mbaya zaidi ya ukosefu wa usalama wa chakula katika kipindi cha miaka minne iliyopita, na kwamba juhudi za makusudi na dharura zinahitajika ili kuyanusuru maisha ya watu hao.

Amesema ukosefu wa usalama na mapigano ndiyo yaliyopelekea kutokea hali hiyo ya kuogofya, na kwamba jamii ya kimataifa inapaswa kuhakikisha kuwa watu milioni 1.9 wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanafikishiwa msaada wa chakula haraka iwezekanavyo ili kuiondoa nchi hiyo katika hatari ya mgogoro mkubwa wa kibinadamu.

Makundi ya waasi yamesababisha ukosefu mkubwa wa usalama CAR

Mwezi Septemba mwaka huu, Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) iliripoti kuwa, hali ya wakazi wa mji wa Alindao wa kusini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati ni mbaya sana kutokana na mapigano yanayoendelea baina ya makundi ya waasi. 

Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ni miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani, ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé kufuatia hujuma ya waasi wa Seleka.

Tangu wakati huo hadi hivi sasa nchi hiyo imekuwa uwanja wa mapigano ya kila uchao kati ya makundi hasimu, hususan lile la Kikristo la Anti-Balaka na kundi la Seleka.