Dec 21, 2018 14:48 UTC
  • Uganda yachukua tahadhari kuhusu Ebola kabla ya uchaguzi  DRC

Uganda imeongeza kiwango cha tahadhari kuhusu ugonjwa wa Ebola, ili kukabiliana na wimbi tarajiwa la wakimbizi iwapo vurugu zitaibuka katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.

Waziri wa afya wa Uganda Bibi Ruth Aceng amesema, hatua za kinga zimechukuliwa na watu wote watakaoingia nchini humo watapimwa ili kuhakikisha hawana ugonjwa wa Ebola. 

Naye mjumbe wa Shirika la Afya Duniani nchini Uganda Bw. Yonas Woldemariam amesema, juhudi maradufu zimefanywa kabla ya uchaguzi ili kuzuia ugonjwa wa Ebola kuingia nchini Uganda. Uchaguzi mkuu wa DRC uliokuwa ufanyike Jumapili Disemba 23 umeahirishwa kwa wiki moja yaani hadi tarehe 30 mwezi huu.

Uchunguzi wa wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na Ebola


Hadi kufikia tarehe 27 Novemba 2018, kulikuwa kumeripotiwa kesi 422 za Ebola, 375 kati ya hizo zikiwa zimethibitishwa na 47 ni za kudhaniwa katika mlipuko wa hivi karibuni wa Ebola DRC. Hadi tarehe hiyo, watu 242 walisharipotiwa kufariki dunia huko Kivu Kaskazini na Ituri.

Mfumuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za magharibi mwa Afrika za Guinea, Liberia na Sierra Leone.
 

Tags