Dec 28, 2018 03:03 UTC
  • Wagonjwa 24 wa Ebola watoroka kituo cha matibabu Beni, Kongo DR

Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza habari ya wagonjwa 24 walioambukizwa ugonjwa hatari wa Ebola kutoroka kituo cha matibabu mjini Beni, mashariki mwa nchi.

Msemaji wa wizara hiyo, Jessica Ilunga jana Alkhamisi aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa, 17 miongoni mwa waliotoroka katika kituo hicho cha matibabu wamethibitika kuwa wana kirusi hicho hatari, huku saba wakiwa bado hawajafanyiwa vipimo.

Inaarifiwa kuwa, washukiwa hao wa Ebola walitoroka baada ya kituo hicho kushambuliwa na watu wanaopinga kuakhirishwa uchaguzi mkuu katika mji huo.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo CENI Jumatano iliyopita ilitangaza kuwa imeakhirisha uchaguzi wa rais na wa bunge uliopangwa kufanyika Jumapili ya tarehe 30 mwezi huu hadi mwezi ujao wa Machi, katika miji mitatu ya Beni, Butembo na Yumbi kutokana na homa ya Ebola na ghasia za kikabila. 

Chanjo ya Ebola

Hadi kufikia tarehe 27 Novemba 2018, kulikuwa kumeripotiwa kesi 422 za Ebola, 375 kati ya hizo zikiwa zimethibitishwa na 47 ni za kudhaniwa. Hadi tarehe hiyo, watu 242 walisharipotiwa kufariki dunia huko Kivu Kaskazini na Ituri.

Mripuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za magharibi mwa Afrika za Guinea, Liberia na Sierra Leone.

Tags