Jeshi la Sudan: Hatutaruhusu nchi isambaratike kutokana na machafuko
(last modified Thu, 31 Jan 2019 14:55:27 GMT )
Jan 31, 2019 14:55 UTC
  • Jeshi la Sudan: Hatutaruhusu nchi isambaratike kutokana na machafuko

Jeshi la Sudan limesema kuwa halitaruhusu nchi isambaratike kufuatia maandamano ya nchi nzima yanayoendelea sasa huku Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo akitahadharisha juu ya kuwepo njama ya kuchochea hali ya mchafukoge nchini humo.

Ni wiki kadhaa sasa Sudan imegubikwa na maandamano na ghasia huku wafanya maandamano wakisisitiza kuwa utawala wa miongo mitatu wa Rais Omar al Bashir inapasa ufikie kikomo. Maandamano nchini Sudan awali yalichochewa na hatua ya serikali ya kupandisha mara tatu bei ya mkate; hatua iliyochochea moto wa maandamano dhidi ya serikali karibu katika miji yote ya nchi hiyo. Mkuu wa majeshi ya Sudan Jenerali Kamal Abdul-Maarouf amesema kuwa vikosi vya ulinzi viko tayari kukabiliana na yoyote anayevuruga usalama wa watu wa Sudan.

Rais Omar al Bashir anayeitawala Sudan kwa miongo mitatu sasa

Amesema hawataruhusu Sudan isamabaratike na kutumbukia kwenye hali ya mchafukoge. Mkuu wa majeshi ya Sudan ameyasema hayo katika mkutano mjini Khartoum na maafisa wa ngazi ya juu wa jeshi. Jumanne wiki hii pia kulitolewa tahadhari kama hii na Essameddine Mubarak Naibu Mkuu wa Majeshi wa Sudan ambaye alibainisha kuwa, vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo viko tayari kupambana na kitisho chochote dhidi ya Sudan.

 

 

Tags