Shambulizi la kigaidi laua askari kadhaa wa Ethiopia nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51293-shambulizi_la_kigaidi_laua_askari_kadhaa_wa_ethiopia_nchini_somalia
Mripuko wa bomu lililokuwa limetegwa garini umeua watu kadhaa wakiwemo wanajeshi wa Ethiopia huko kusini mwa Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 02, 2019 21:57 UTC
  • Shambulizi la kigaidi laua askari kadhaa wa Ethiopia nchini Somalia

Mripuko wa bomu lililokuwa limetegwa garini umeua watu kadhaa wakiwemo wanajeshi wa Ethiopia huko kusini mwa Somalia.

Meja Nur Abdullahi, ofisa wa ngazi za juu wa polisi katika eneo hilo amesema basi dogo lililokuwa limebeba mboga za majani liliripuka nje ya kambi ya jeshi la Ethiopia katika mji wa Bardheere kusini mwa Somalia na bila kutaja idadi, amesema askari kadhaa wa Ethiopia wameuawa na wengine kujeruhiwa. 

Mzee mmoja aliyeshuhudia tukio hilo amesema watu kumi wakiwemo wanajeshi wa Ethiopia wanaohudumu chini mwa mwavuli wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) na raia wameuawa katika mripuko huo.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab kwa upande wake limedai kuwa limeua wanajeshi 16 wa Ethiopia katika shambulizi hilo la bomu la jana Jumamosi.

Askari wa AMISOM nchini Somalia

Haya yanajiri siku chache baada ya jeshi la Ethiopia kutangaza kuwa linajiandaa kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya maficho ya al-Shabaab baada ya kundi hilo kushambulia msafara wa magari ya jeshi la Ethiopia karibu na mji wa Burhakaba kusini mwa Somalia.

Katika hali ambayo taarifa ya jeshi la Ethiopia ilisema wanajeshi wake waliweza kuzuia shambulizi hilo na kurudi kambini salama, lakini kundi  hilo la ukufurishaji lilitangaza kuwa limewaua wanajeshi zaidi ya 50 wa Ethiopia.