Mripuko wa bomu wauawa watu 3 garini DRC
Watu watatu wameuawa katika mripuko wa kile kinachoaminika kuwa bomu la kutegwa garini mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Evariste Manegabe, afisa wa serikali ya mtaa katika mkoa wa Kivu Kusini amesema waliouawa kwenye mripuko huo wa jana Ijumaa ni wanawake wawili na mwanamme mmoja waliokuwa kwenye gari hilo, katika mji wa Bukavu. Amesema kuwa visa vya aina hii ni nadra kuripotiwa katika eneo hilo na kwamba wameanzisha uchunguzi kubaini kiini cha mripuko huo na malengo ya waliohusika.
Duru za polisi katika mkoa wa Kivu Kusini zimedokeza kuwa, mripuko huo ulisababishwa ima na bomu la kutegwa garini au mmoja kati ya watu waliokuwa kwenye gari hilo alikuwa amebeba mada za miripuko.
Eneo la Kivu Kusini sawa na maeneo mengine ya mashariki mwa Kongo DR limekuwa likishuhudia machafuko na mapigano ya mara kwa mara kati ya maafisa usalama na waasi.
Zaidi ya watu 30 waliuawa mwishoni mwa mwaka uliopita, katika mji wa Eringeti, yapata kilomita 55 kaskazini mwa mji wa Beni, uliopo karibu na mpaka wa DRC na Uganda.
Januari mwaka huu, Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka lilisimamisha huduma zake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya msafara wao kushambuliwa na maafisa wake wawili kutekwa nyara mashariki mwa nchi.