Feb 13, 2019 07:43 UTC
  • Ripoti: Wanawake Kongo DR wananunua chanjo ya Ebola kwa ngono

Vyanzo mbalimbali ya habari vimeripoti kuwa, wanawake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanalazimika kufanya ngono mkabala wa kupewa chanjo ya ugonjwa hatari wa Ebola, ambao umeua mamia ya watu kufikia sasa.

Gazeti la The Guardian limenukuu ripoti ya utafiti uliofanywa na Jopokazi la Kitaifa Kuhusu Maambukizi ya Ebola iliyofichua kuwa, aghalabu ya wanawake wanaoishi katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na virusi hivyo wanalazimika kununua chanjo ya Ebola kwa kushiriki ngono na maafisa husika.

Trina Helderman, Mshauri Mkuu wa Afya na Lishe wa asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Medair amezikosoa taasisi za kibinadamu kwa kushindwa kuwalinda wanawake na wasichana wanaolazimika au kulazimishwa kununua kinga hiyo muhimu mkabala wa kudhalilishwa kingono.

Wizara ya Afya ya DRC imewataka wananchi kuripoti tukio lolote la kuitishwa pesa au wanawake kulazimishwa kushiriki ngono mkabala wa kupewa chanjo ya Ebola.

Maafisa wa Afya wakitoa chanjo ya Ebola mjini Beni, DRC

Hii ni katika hali ambayo, Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kuwa, idadi ya watu waliofariki dunia kwa maradhi ya Ebola tangu yaibuke upya mwezi Agosti mwaka jana katika mkoa wa Kivu Kaskazini ambao unapakana na Uganda na Rwanda ni 510.

Taarifa ya Wizara ya Afya ya nchi hiyo ya katikati mwa Afrika imesema kuwa, mpango wa chanjo dhidi ya maradhi hayo umeokoa maisha ya watu 76,425.

 

Tags