Mar 01, 2019 07:57 UTC
  • Kituo cha kutibu Ebola Butembo, DRC chahujumiwa

Kituo cha kutibu Ebola huko Butembo, jimbo la Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kimehujumiwa na watu wasiojulikana.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Alhamisi  na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF ambalo limebainisha masikitiko yake kufuatia hujuma hiyo.

Taarifa hiyo imesema shambulio hilo lilijiri Jumatano kwenye kituo hicho kinachoendeshwa na Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, MSF  ambapo afisa mmoja wa polisi aliuawa na kituo kuchomwa moto. Shirika la MSF limetangaza kusimamisha shughuli zake kufuatia hujuma hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore ametuma salamu za rambirambi kwa familia na ndugu wa mtumishi huyo pamoja na MSF akisema kituo hicho kinahudumia watoto na familia zao.

Ameongeza kuwa kila siku, wafanyakazi wa UNICEF na wadau wetu wakiwemo wahudumu wa afya kwenye vituo vya matibabu na jamii wanafanya juhudi za kishujaa kuokoa maisha ya watoto na watu wazima ambao wameathiriwa na Ebola.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNICEF amesema njia pekee ya kutokomeza Ebola ni kwa wahudumu wa afya, UNICEF, wadau kuweza kufanya kazi kwa usalama kwenye jamii zilizokumbwa na ugonjwa huo, yakiwemo maeneo  ya ndani zaidi.

Kituo cha afya cha kuwatibu wagonjwa wa Ebola, DRC

Amesisitiza kuwa vituo vya afya katu havipaswi kuwekwa rehani kwa kukosesha usalama mashariki mwa DRC.

Zaidi ya watu 800 nchini DRC wameathirika na Ebola katika mlipuko huu wa hivi kairbuni zaidi ulioanza mwezi Agosti mwaka jana ambapo 500 kati yao wamefariki dunia.

Hata hivyo kwenye maeneo kama Mangina, Beni, Komanda ugonjwa  umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa ambapo zaidi ya watu 250 wamepona na 80,0000 wamepatiwa chanjo dhidi ya Ebola.

 

Tags