Mar 04, 2019 02:40 UTC
  • El Baradei akosoa ukandamizaji dhidi ya wafungwa wa kisiasa Misri

Makamu wa zamani wa rais wa Misri amekosoa ukandamizaji unaofanywa na serikali ya nchi hiyo dhidi ya wafungwa wa kisiasa ikiwa ni pamoja na kuzuia familia za wafungwa hao kuwatembelea korokoroni kwa kipindi kirefu.

Muhammad el Baradei amekosoa hatua ya serikali ya Misri ya kuzuia familia ya rais aliyeondolewa madarakani Muhammad Mursi, viongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin na wafungwa wengine wa kisiasa kutembelea jamaa zao wanaoshikiliwa jela.

Mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel amekemea hatua ya kuzuia familia za wafungwa wa kisiasa kutembelea ndugu zao wanaoshikiliwa katika korokoro za serikali ya Misri kwa miezi au hata miaka kadhaa na kukitaja kitendo hicho kuwa ni kinyume cha sheria na maadili ya kibinadamu. Amesisitiza kuwa, jambo hilo halipasi kuruhusiwa.

El Baradei ambae aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia amesema anashangazwa na hasira za serikali ya Cairo pale inapokosolewa kuwa inakiuka haki za binadamu na hali mbaya inayotawala jela na korokoro za nchi hiyo.

Muhammad el Baradei

El Baradei ameitaka serikali ya Misri kutoa huduma ya matibabu kwa Mohamed Beltagy ambaye ni miongoni mwa vinara wa harakati ya Ikhwanul Muslimin wanaoshikiliwa katika korokoro za nchi hiyo ambaye amepatwa na maradhi ya kiharusi kutokana na kutelekezwa na vyombo vya dola.

Jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu zinasema kuwa, jela za Misri hususan ile ya El ʿAqrab zimejaa idadi kubwa ya vinara wa harakati ya Ikhwanul Muslimin na wafungwa wengine wengi wa kisiasa na kwamba wanasulubiwa na kupewa mateso.  

Tags