Mar 30, 2019 07:56 UTC
  • Kesi mpya za ugonjwa wa Ebola zaripotiwa Kongo DR

Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imethibitisha kesi nyingine 15 za ugonjwa hatari wa Ebola.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, kesi hizo mpya zilizoripotiwa jana Ijumaa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kuthibitishwa ndani ya siku moja tangu wimbi jipya la ugonjwa huo lilipoikumba nchi hiyo mwezi Agosti mwaka jana 2018.

Kesi hizo mpya zimeripotiwa siku moja baada ya kesi nyingine 15 za ugonjwa huo hatarishi ambao umeua mamia ya watu kuthibitishwa katika nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika.

Jana Ijumaa pia, Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ilisema mripuko wa ugonjwa huo hatari umeshaua watu 660 na kuambukiza wengine 399 tangu mwezi Agosti mwaka jana hadi hivi sasa.

Vituo vitano vya kutoa chanjo ya Ebola vimeshambuliwa tangu mwezi jana hadi sasa huko DRC

Wiki iliyopita, Shirika la Afya Duniani WHO lilitoa wito wa kukabiliana na hali ya mripuko wa homa ya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako watu takriban 1,000 wameambukizwa ugonjwa huo.

Mripuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za magharibi mwa Afrika za Guinea, Liberia na Sierra Leone.

Tags