Apr 14, 2019 16:53 UTC
  • Zaidi ya watu 2000 wahukumiwa kifo nchini Misri

Mahakama za Misri zimetoa adhabu ya kifo kwa watu elfu mbili na 159 nchini humo.

Shirika la habari la AFP limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, makundi ya haki za binadamu ya Misri yameripoti kwamba baina ya mwaka 2014 hadi 2018 yaani katika kipindi cha miaka minne, mahakama za Misri zimewahukumu adhabu ya kifo watu 2,159.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, makundi ya haki za binadamu ya ndani ya Misri yameripoti kwamba, watu 92 kati yao wamehukumiwa kifo katika miaka ya 2017 na 2018. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa, watu 15 wameshahukumiwa kifo nchini Misri.

Mahakama ya kuwahukumu wafuasi wa Ikhwanul Muslimin nchini Misri

 

Makumi ya watu wako katika korokoro mbalimbali za Misri wakisubiri kutekelezewa hukumu zao. Kwa mujibu wa familia za watu hao, athari za mateso zinaonekana waziwazi katika miili ya jamaa zao ambao wametekelezewa adhabu ya kifo kwa tuhuma kama za kushiriki katika vitendo vya kigaidi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, huku za kifo zinatolewa kwa baadhi ya watuhumiwa ambao wamelazimishwa kukiri makosa wasioyofanya ili kujiepusha na mateso.

Maelfu ya wafuasi wa Ikhwanul Muslimin wa Misri wametiwa mbaroni katika miaka ya hivi karibuni na kuhukumiwa adhabu kali hasa kifo.

Wengi wa Wamisri wanaohukumiwa adhabu ya kifo nchini humo ni wanachama wa Ikhwanul Muslimin.

Tags