CAR yatangaza maombolezo ya kitaifa baada ya mauaji ya umati
Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia Alhamisi baada ya watu zaidi ya 50 kuuawa kwa umati Jumanne karibu na mpaka wa nchi hiyo na Chad.
Rais Faustin-Archange Touadera wa CAR ametoa tangaza hilo huku akisema mauaji hayo yametekelezwa na wanamgambo wanaojulikana kama 3R. Aidha amewataka viongozi wa kundi hilo kuwakabidhi wale wote waliohusika moja kwa moja na mauaji hayo.
Kufuatia mauaji hayo, askari wa Umoja wa Mataifa wameimarisha doria katika mji wa Paoua wa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Kwa mujibu wa maafisa wa Umoja wa Mataifa, wanamgambo wa 3R waliwaita wakaazi wa vijiji kadhaa katika eneo hilo kwa ajili ya mkutano na hapo wakaanza kufyatua risasi kiholela. Sababu hasa ya mauaji hayo haijaweza kubainika.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuchunguza mauaji hayo na kuwafikisha kizimbani wahusika.
Machafuko huko Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) yalizuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé. Baada ya Rais Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya Waislamu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.