May 31, 2019 02:28 UTC
  • Jeshi la DRC laua wanamgambo 26 katika mji ulioathiriwa na Ebola

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza habari ya kuua wanamgambo 26 karibu na mji wa Beni ulioathiriwa na ugonjwa hatari wa Ebola, mashariki mwa nchi.

Msemaji wa jeshi la Kongo DR, Jenerali Leon-Richard Kasonga amesema wanamgambo hao waliuawa katika makabiliano na askari wa serikali jana Alkhamisi, katika kijiji cha Ngite nje kidogo ya mji wa Beni.

Amesema wanamgambo hao wa ADF walianza kuwafyatulia risasi maafisa usalama ndipo wakajibu mapigano kukabiliana nao vikali. Hata hivyo taarifa ya afisa huyo haijaeleza iwapo kuna askari wa DRC aliyeuawa au kujeruhiwa katika makabiliano hayo ya jana Alkhamisi.

Mapema mwezi huu, watu tisa waliripotiwa kupoteza maisha katika mapigano baina ya askari wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wanamgambo waliobeba silaha katika mji wa Butembo ambao pia umeathiriwa na ugonjwa hatari wa Ebola.

Kliniki ya kutibu Ebola iliotekeketezwa na waasi mashariki mwa DRC

Juhudi za kupambana na ugonjwa wa Ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeendelea kukabiliwa na vizingiti kutokana na makundi hayo ya wanamgambo kushambulia vituo vya afya vinavyotoa matibabu kwa wagonjwa wa maradhi hayo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, watu zaidi ya 1,200 wameaga dunia kutokana na maradhi ya Ebola nchini humo tangu ugonjwa huo hatari uibuke upya Agosti mwaka jana.

 

Tags