Waandamanaji waliouawa na maafisa usalama Sudan wapindukia 108
Idadi ya watu waliouawa katika wimbi jipya la ukatili na utumiaji wa nguvu kupita kisiasa wa maafisa usalama wa Sudan dhidi ya waandamanaji wanaotaka kukabidhiwa madaraka kwa utawala wa kiraia imepindukia watu 100.
Mashirika yanayoongoza maandamano hayo ya wananchi yameripoti kuwa, idadi ya watu waliouawa tangu maafisa usalama waanze kuyashambulia makundi ya waandamanaji kwa risasi hai Jumapili iliyopita hadi sasa ni 108.
Nayo Kamati ya Madaktari ya Sudan imesema kuwa, idadi isiyojulikana ya miili imeopolewa kutoka Mto Nile, mbali na maiti 40 zilizokuwa zimeopolewa hapo kabla kutoka kwenye mto huo.
Makundi hayo ya kiraia yanayoongoza maandamano ya wananchi yamebainisha kuwa, watu zaidi 500 wamejeruhiwa na maafisa usalama katika wimbi hili jipya la mashambulizi ya maafisa usalama.
Jumapili iliyopita jeshi la Sudan, chini ya Baraza la Kijeshi linalotawala nchi, liliwashambulia raia waliokuwa katika mgomo wa kuketi chini mbele ya makao makuu ya kamanda wa jeshi la nchi hiyo mjini Khartoum.
Maandamano ya hivi karibuni yalishtadi baada ya kufeli mazungumzo kati ya Baraza la Kijeshi la Mpito na Muungano wa Uhuru na Mabadiliko, kuhusiana na namna ya muundo wa baraza la utawala na namna ya kukabidhi madaraka kwa raia.
Mauaji hayo yamefanyika baada ya vinara wa baraza hilo kutembelea nchi za Saudi Arabia, Imarati na Misri na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hizo.