Jun 10, 2019 02:36 UTC
  • Kesi nyingine elfu moja za Ebola zagunduliwa DRC

Hujuma na mashambulizi dhidi ya makundi ya madaktari Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni kikwazo kikubwa cha kupambana na ugonjwa hatari wa Ebola nchini humo.

Wizara ya Afya ya nchi hiyo imesema katika taarifa yake kwamba machafuko na hutuma dhidi ya makundi ya madaktari yanakwamisha zoezi la kupambana na ugonjwa wa Ebola na hivi sasa kesi 1000 za ugonjwa huo hatari zimeripotiwa katika kipindi cha wiki 33 zilizopita.

Taarifa ya wizara hiyo imesema kuwa shambulizi lolote dhidi ya timu ya madaktari na hujuma yoyote ile dhidi ya watoa huduma za tiba hushadidisha maradhi ya Ebola na kukwamisha kazi zao kwa muda wa siku 10 hadi 15.

Makundi yenye silaha hushambulia mara kwa mara vituo vya matibabu na kuwaua maafisa wa tiba wanaotoa huduma za kupambana na ugonjwa wa Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. 

Madaktari hutoa huduma mbalimbali za kukabiliana na maradhi hatari ya Ebola ikiwemo chanjo

 

Hii ni katika hali ambayo siku chache zilizopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema karibu robo ya watu walioambukizwa Ebola huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamkini hawajui kwamba wanaugua ugonjwa huo hatari.

Katika taarifa yake WHO ilisema kuwa mtu mmoja kati ya kila watu wanne mashariki mwa DRC, ameambukizwa ugonjwa hatari wa Ebola lakini hafahamu.

WHO imesema hilo wakati huu inapoendelea kusaidia kupambana na maambukizi ya Ebola hasa mjini Beni, ambapo watu zaidi ya 2,000 wameambukizwa na wengine 1,357 wamepoteza maisha tangu mwezi Agosti mwaka 2018.

Hivi karibuni pia Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ilitahadahrisha kuhusu tishio la ugonjwa hatari wa Ebola kuenea katika nchi za jumuiya hiyo.

Tags