Jun 12, 2019 12:58 UTC
  • Ebola yaua katika kesi ya kwanza ya ugonjwa huo nchini Uganda

Kijana aliyekuwa na umri wa miaka mitano ameaga dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola, hii ikiwa ni kesi ya kwanza ya maradhi hayo hatari kuthibitishwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Duru za habari zimearifu kuwa, kijana huyo alikuwa akitibiwa katika kituo kimoja cha afya mjini Kasese, katika mpaka wa magharibi wa Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Jana jioni, Shirika la Afya Duniani WHO bila kutoa maelezo ya kina, lilithibitisha kesi ya kwanza ya ugonjwa huo nchini Uganda.

Haya yanaripotiwa chini ya mwezi mmoja baada ya Uganda kutangaza kuwa imechukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kuzuia ugonjwa hatari wa Ebola usiingie nchini humo ukitokea nchi jirani ya DRC, hasa kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kumiminika nchini Uganda. 

Hii ni katika hali ambayo siku chache zilizopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema karibu robo ya watu walioambukizwa Ebola huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yumkini hawajui kwamba wanaugua ugonjwa huo hatari.

Utoaji wa chanjo ya Ebola DRC

Mashambulizi dhidi ya makundi ya madaktari wanaotibu Ebola huko Kongo DR yanakwamisha zoezi la kupambana na ugonjwa huo ambao umeua zaidi ya watu 1,300 tokeo ulipuke upya nchini humo mnamo Agosti mwaka jana.

Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC imetahadharisha kuhusu tishio la ugonjwa hatari wa Ebola kuenea katika nchi za jumuiya hiyo.

Tags