Jun 17, 2019 12:31 UTC
  • Mgonjwa mwenye dalili za Ebola Kenya awekwa karantini

Mgonjwa anayeshukiwa kuwa na Ebola nchini Kenya amewekwa katika karantini katika Hospitali ya Kericho magharibi mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Gavana wa Kaunti ya Kericho, mgonjwa huyo, ambaye ni mwanamke alifikishwa hospitalini jana Jumapili akiwa na dalili zinazowapata wagonjwa wa Ebola.

Maafisa wa afya katika Kaunti ya Kericho wamesema kuwa alikuwa amesafiri kutoka Malaba eneo la mpaka kati ya Kenya na Uganda.

Hakuna ripoti yeyote iliyotolewa ya kuwepo kwa ugonjwa wa Ebola karibu na mpaka wa Malaba ingawa watu wawili wamefariki dunia kutokana na Ebola eneo la Magaharibi mwa Uganda.

Sampuli za damu za mgonjwa huyo zimechukuliwa na kupelekwa katika  Taasisi ya Utafiti wa Tiba ya Kenya (KEMRI) mjini Nairobi kwa ajili ya kufanyiwa vipimo.

Mgonjwa huyo alikwenda hospitali binafsi siku ya Jumapili akiwa na homa, maumivu ya kichwa, maumivu ya viungo, maumivu ya koo na alikua akitapika.

Alitibiwa malaria kwenye hospitali ndogo lakini hali yake ikazidi kuwa mbaya.

Eneo la kuwatibu wagonjwa wa Ebola nchini DRC

Alifanyiwa tena kipimo cha malaria na majibu yalionyesha hana malaria. Kutokana na hali hiyo wahudumu wa afya walimpa rufaa kwenda hospitali ya Kaunti ya Kericho ambayo ina uwezo wa kuweka karantini. Hata hivyo sampuli za mgonjwa huyo baada ya vipimo zimeonyesha kuwa hana maambukizo ya homa hiyo hatari. 

Haya yanajiri baada ya Kamati ya dharura ya Shirika la Afya Duniani, WHO kutangaza kuwa mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ni tishio la afya nchini humo na nchi jirani. WHO imesema Ebola kwa sasa si tishio la kimataifa. Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus  amesema tangu mlipuko wa maradhi hayo uanze mwezi Agosti mwaka jana hadi leo, watu 2108 wameambukizwa Ebola nchini DRC na kati ya hao 1411 wamefariki dunia.

Tags