Wanajeshi 18 wa Niger wauawa katika hujuma dhidi ya kambi yao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54506-wanajeshi_18_wa_niger_wauawa_katika_hujuma_dhidi_ya_kambi_yao
Kwa akali askari 18 wameuawa baada ya watu waliojizatiti kwa silaha kushambulia kambi ya jeshi magharibi mwa Niger.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 02, 2019 07:30 UTC
  • Wanajeshi 18 wa Niger wauawa katika hujuma dhidi ya kambi yao

Kwa akali askari 18 wameuawa baada ya watu waliojizatiti kwa silaha kushambulia kambi ya jeshi magharibi mwa Niger.

Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, shambulizi hilo lilifanyika jana Jumatatu nyakati za alasiri karibu na mji wa Inates ulioko mpakani mwa nchi hiyo na Mali.

Jeshi la Niger halijatoa taarifa ya kuthibitisha kutokea shambulizi hilo, na pia hakuna kundi la kigaidi limetangaza kuhusu nalo hadi sasa.

Hata hivyo, Zakari Insa ambaye ni ndugu ya mmoja wa wanajeshi waliouawa pamoja na Souley Marou, mkazi wa eneo hilo wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa ni kweli shambulizi hilo limefanyika na kwamba wanajeshi 18 wa serikali wameuawa. 

Haya yanajiri katika hali ambayo, mwezi uliopita wa Juni serikali ya Niger ilitangaza kurefusha muda wa hali ya hatari katika maeneo ya mashariki na magharibi mwa nchi hiyo kwa miezi mingine mitatu; kwa lengo la kudhamini usalama wa raia na mali zao na vile vile kwa ajili ya kurejesha amani na utulivu katika maeneo hayo.

Magaidi wanaendeleza harakati zao Niger licha ya uwepo wa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa

Mwezi mmoja kabla ya tangazo hilo, kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) lilitangaza kuhusika na shambulio dhidi ya msafara wa magari ya jeshi la Niger ambalo liliua askari 28 wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Niger ambayo ni moja ya nchi masikini zaidi duniani inaandamwa na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na magenge ya ndani na nje ya nchi.