Jul 17, 2019 12:28 UTC
  • WHO yatahadharisha kuhusu hatari ya kuenea homa ya Ebola huko Kongo DR

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa mlipuko wa homa ya Ebola ulioukumba mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huwenda ukawa na athari mbaya sana.

Maafisa wa afya katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo wiki hii wameripoti kuwa mgonjwa wa kwanza  ambaye alikuwa ameambukizwa virusi vya homa hatari ya Ebola katika mji mkubwa zaidi mashariki mwa nchi hiyo wa Goma ameaga dunia.

Kuaga dunia  mtu huyo aliyetajwa kuwa ni mchungaji wa kanisa kumezidisha wasiwasi kuhusu uwezekano wa kueneza zaidi maambukizo ya Ebola huko Kongo. Wakati huo huo washiriki katika mkutano wa dharura wa WHO uliofanyika Jumatatu wiki hii katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametilia mkazo udharura wa kukomesha maambukizo ya virusi vya homa hatari ya Ebola. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa watu karibu 2,500 wameambukizwa virusi vya Ebola Kongo DR na 665 wameaga dunia kwa ugonjwa huo. Marc Lowcock mmoja wa maafisa katika mkutano huo wa dharura wa WHO amesema inaonekana kuwa ukosefu wa vyanzo vya fedha na hali mbaya ya usalama mashariki mwa Kongo ndio vitisho vikuu vinavyokwamisha kampeni ya kupambana na maambukizo ya Ebola. 

Kwa upande wake Dakta Tedros Adhanom Gebreyesus  Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani ameeleza kuwa jitihada za kutokomeza maambukizo ya Ebola zimepata pigo jingine baada ya taarifa za kutambuliwa mgonjwa wa kwanza aliyeambukizwa virusi vya homa hiyo katika mji wa Goma. 

Dr Tedros Adhanom Gebreyeyus Mkurugenzi wa WHO
 

 

 

Tags