Aug 03, 2019 11:44 UTC
  • Congo DR yazidisha jitihada za kudhibiti Ebola mashariki mwa nchi hiyo

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeanzisha juhudi kubwa za kudhibiti ugonjwa hatari wa virusi vya Ebola huko mashariki mwa nchi hiyo baada ya mchimba migodi mmoja aliyekuwa na familia kubwa kuaga dunia kutokana na homa ya ugonjwa huo katika mji wa Goma.

Ijumaa ya jana serikali ya Congo DR ilitangaza kuwa mke wa mchimba migodi huyo aliyefariki dunia pia amegundulika kuwa na virusi vya Ebola katika mji huo ulioko kwenye mpaka wa Congo na Rwanda. Mratibu wa serikali ya Congo kuhusu maambukizi ya Ebola, Jean-Jacques Muyembe, amesema mtoto mmoja kati ya kumi wa familia hiyo pia amelazwa akihofiwa kuambukizwa virusi hivyo hatari.

Ugonjwa huo wa Ebola umekwishaua watu wasiopungua 1800 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu uliporipuka tena yapata mwaka mmoja uliopita.

Ugonjwa wa Ebola unaendela kuua watu Congo

 

Ripoti ya kugunduliwa kesi zaidi za maambukizi ya Ebola katika mji wa Goma inazidisha wasiwasi wa kueneza zaidi ugonjwa huo kwenye eneo hilo lenye idadi kubwa ya watu ambalo liko umbali wa kilomita zaidi ya 350 kutoka mahaka ugonjwa huo ulipogundulika kwa mara ya kwanza katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mfumuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa Afrika.

Tags