Uganda yawapa chanjo ya surua na polio watoto milioni 18
Wizara ya Afya ya Uganda kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani WHO zinatazamiwa kuanza kuwapa chanjo za surua (measles) na ugonjwa wa kupooza (polio) watoto milioni 18 wenye chini ya umri wa miaka 15 nchini humo.
Shughuli ya kutoa chanjo hizo inatazamiwa kuanza leo Jumatano na itaendelea kwa muda wa siku tano. Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya Wizara ya Afya ya Uganda na Shirika la Afya Duniani WHO, watoto milioni 18, sawa na asilimia 43 ya idadi jumla ya wananchi wote wa Uganda watapewa chanjo hizo za surua, polio na virusi vya rubella.
Ruth Aceng, Waziri wa Afya wa Uganda amewataka wazazi na watu wenye kusimamia watoto kuhakikisha kuwa watoto wote wanapewa chanjo hizo, ikiwa ni hatua ya tahadhari kabla ya hatari.
Naye Yonas Tegegn Woldermariam, mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani nchini Uganda amewahakikishia wananchi wa Uganda kuwa chanjo hizo ni salama, zenye manufaa na zinazotolewa bila malipo.
Katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ugonjwa wa surua umeua watu zaidi ya elfu nne tangu mwezi Januari mwaka huu, ambapo takribani asilimia 90 ya vifo hivyo ni watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.