Mripuko wa bomu waua askari wa Ufaransa nchini Mali
Mwanajeshi wa Ufaransa ameuawa katika mripuko wa bomu la kutegwa kando ya barabara karibu na eneo la Menaka mashariki mwa Mali.
Ofisi ya Rais wa Ufaransa imethibitisha kifo cha Koplo Ronan Pointeau, askari wa kulinda amani wa Ufaransa katika eneo la Menaka, baada ya gari la deraya alilokuwa akiliendesha kuripukiwa na bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ametoa mkono wa pole kwa familia ya askari huyo na kusema kuwa, "Fikra zangu ziko pamoja na Pointeau na wanajeshi wenzake ambao wanajitolea muhanga kupambana na ugaidi katika eneo la Sahel."
Kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) limetangaza kuhusika na hujuma hiyo, pamoja na shambulizi la Ijumaa lililoua makumi ya askari wa Mali.
Ijumaa iliyopita Jeshi la Mali lilitangaza kuwa, wanajeshi wake 53 na raia mmoja wameuawa katika hujuma iliyofanywa na kundi la watu waliokuwa na silaha dhidi ya kambi moja ya jeshi katika eneo la Indelimane mkoa wa Menaka ulioko kaskazini mwa nchi hiyo karibu na mpaka wa Mali na Niger.
Machafuko Mali yalianza mwaka 2012 ambapo magenge mbalimbali ya kigaidi yamejitokeza na yanafanya mashambulizi na mauaji ya mara kwa mara nchini humo.
Umoja wa Mataifa una wanajeshi wake nchini humo wanaojulikana kwa jina la MINUSMA. Wanajeshi wa Ufaransa nao wako nchini humo tangu mwaka 2013 lakini hadi leo wameshindwa kuleta utulivu na kuzuia mashambulizi ya kigaidi nchini humo.