Uchaguzi wa rais Guinea-Bissau wagubikwa na ghasia
Uchaguzi wa rais nchini Guinea-Bissau umemalizika kwa kushuhudiwa ghasia na mapigano kutokana na upande wa upinzani kuituhumu serikali kuwa imefanya uchakachuaji.
Kwa mujibu wa habari, wapinzani wa serikali wamemkosoa Rais José Mário Vaz kwa kufanya uchakachuaji kwa maslahi yake. Baada ya kutangazwa matokeo ya awali ya uchaguzi huo, wakazi wa Bissau, mji mkuu wa nchi hiyo wamemiminika mabarabarani katika maandamano yaliyoingiliwa na wafuasi wa Rais José Mário Vaz na kupelekea kuibuka mapigano baina yao. Hii ni katika hali ambayo awali rais huyo alikuwa ametangaza kwamba angekubaliana na matokeo yatakayotangazwa na tume ya uchaguzi.
Huku upande wa upinzani ukimkosoa Rais José Mário Vaz kwa kufanya uchakachuaji, nayo kambi ya rais huyo imeelekeza tuhuma kwa upinzani kwamba ulitoa rushwa kwa lengo la kukusanya kura na kutangazwa matokeo kwa maslahi yake. Tangu Guinea-Bissau ipate uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno yaani mwaka 1974 imeshuhudia mapinduzi ya kijeshi na mauaji mengi ya kisiasa. Aidha nchi hiyo maskini ya magharibi mwa Afrika yenye watu milioni moja na nusu, inahesabiwa kuwa moja ya nchi maskini zaidi duniani.