Sharti la serikali ya Ufaransa kuzisaidia kijeshi nchi za magharibi mwa Afrika
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amewataka viongozi wa magharibi mwa Afrika kupinga kuongezeka hisia dhidi ya Ufaransa katika eneo iwapo wanataka Paris iendelee na oparesheni zake dhidi ya makundi ya wanamgambo wenye silaha.
Itakumbukwa kuwa Ufaransa ina idadi kubwa ya wanajeshi wanaoendesha oparesheni dhidi ya makundi ya kigaidi huko Mali na katika eneo kuu la Sahel. Licha ya uwepo wa wanajeshi hao wa Ufaransa, lakini hali ya ukosefu wa usalama imekuwa ikizidi kuwa mbaya siku baada ya siku huku wanamgambo wenye mfungamano na makundi ya kigaidi ya al Qaida na Daesh yakizidi kujiimarisha katika eneo la Sahel khususan huko Mali na nchini Burkinafaso.
Serikali ya Ufaransa imekuwa ikikosolewa kuhusu utendaji wa kikosi chake cha wanajeshi 4,500 katika eneo la Sahel kwa kushindwa kurejesha amani na uthabiti katika eneo hilo. Rais Macron amewataka viongozi wa nchi za Mali, Niger, Burkina Faso, Chad na Mauritania kutoa maelezo na kuwasilisha rasmi matakwa yao mbele ya Ufaransa na jamii ya kimataifa. Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa Nato mjini London Rais Macron amesema, anataka maelezo ya wazi iwapo viongozi hao wa magharibi mwa Afrika wanataka wanajeshi wa Ufaransa waendelea kuwepo huko Sahel au la.