Waziri Mkuu wa Sudan aazimia kuwaondoa askari wa nchi hiyo Yemen
Waziri Mkuu mpya wa Sudan, Abdalla Hamdok ameeleza juu ya azma ya serikali yake ya kuviondoa kikamilifu vikosi vya askari wa nchi hiyo kutoka Yemen, akisisitiza kuwa taifa lake linapaswa tu kuunga mkono mchakato wa kisiasa wa kuupatia ufumbuzi mgogoro unaoikabili nchi hiyo maskini ya Kiarabu.
Hamdok amesema hayo katika mazungumzo yake na Baraza la Wanafikra la Atlantic la Marekani na kueleza bayana kuwa, "Mgogoro wa Yemen hautaki suluhu ya kijeshi, ama kutoka kwetu au nchi yoyote ile."
Amesema vita vinapaswa kusimamishwa kwa kutumia njia za kisiasa, na kwamba taifa lake litashirikiana na Wayemen kuhakikisha kuwa muafaka na ufumbuzi wa mzozo huo unapatikana.
Haya yanajiri siku chache baada ya Katibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi wa Sudan tawi la kaskazini kutoa wito wa kurejeshwa nyumbani wanajeshi wa Sudan wanaopigana kwa niaba ya Saudi Arabia nchini Yemen.
Upinzani wa Wasudan dhidi ya kutumwa wanajeshi wa Sudan katika vita vya Yemen ulianza katika kipindi cha utawala wa Omar al Bashir na umeshika kasi zaidi baada ya rais huyo wa zamani kuondolewa madarakani.
Mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu, Mohammed Hamdan Dagalo, Naibu Mkuu wa Baraza la Utawala wa Mpito nchini Sudan alisema kuwa askari elfu 10 wa nchi hiyo wameondoka nchini Yemen, ikiwa ni katika awamu ya kwanza ya kuwaondoa wanajeshi hao hatua kwa hatua.
Wakati mgogoro wa Yemen uliposhadidi kati ya mwaka 2016 na 2017, serikali ya Khartoum ilituma wanajeshi 40,000 katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu, kupigana kwa niaba ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia.